Wabunge wa Chadema, John Mnyika kutoka Kibamba na Peter
Msigwa wa Iringa vijijini leo Juni 5, 2018 wameibana serikali bungeni kuhusu
madai ya wananchi hasa viongozi na makada wa chama hicho kubambikiwa kesi na
askari polisi.
Akizungumza bungeni Msigwa alidai kuwa, kuna tabia iliyoibuliwa
na baadhi ya askari polisi ya kuwabambikizia kesi viongozi na makada wa vyama
vya upinzani hasa wa Chadema, na kwamba huwalazimisha
kuhamia chama tawala ili wasibambikiwe kesi.
“Tabia ya polisi kubambikizia kesi, mimi ni muhanga wa kubambikiziwa
kesi, RCO wa Iringa anatabia ya kulazimisha wananchama wa Chadema kuhamia CCM ili
wasibambikiziwe kesi,” alidai Msigwa.
Akijibu swali Msigwa, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi, Eng. Hamad Massauni “madai ya Msigwa amekuwa anayatoa mara kwa mara bungeni
na nilimuomba alete uthibitisho lakini haleti, kwa taarifa zilizopo hadi sasa
hakuna askari polisi aliyekutwa anafanya matendo hayo kinyume na sheria.”
Akiuliza swali la Mbunge wa Tarime Vijijini John Heche,
Mnyika alidai kwamba kuna kesi nyingi wanazobambikiziwa baadhi ya wananchi hasa
kesi za wizi na mauaji, na kuhoji kuwa kwa nini serikali isiwasaidie wahanga wa
vitendo hivyo kwa kuwapatia msaada wa kisheria.
Pia, Mnyika aliitaka serikali kuruhusu Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora iende kufanya uchunguzi katika gereza la Tarime kubaini
watuhumiwa waliobambikiziwa kesi, vile vile alihoji serikali itaanza lini
kulipa fidia watu wanaobambikiziwa kesi ili tabia hiyo ikome.
Akijibu swali la Heche kwa niaba ya Waziri wa Katiba na
Sheria, Naibu Waziri wa Kazi,
Vijana na Ajira, Mhe. Antony Mavunde amesema
“Utaratibu wa kimahakama uko wazi, inapotokea mtu ameshtakiwa
mahakamani, na ikagundulika amebabmbikiziwa kesi inamtaka afungue kesi za
madai, utaratibu upo na watu wafuate sheria.”
