Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job
Ndugai amewajibu watu wanaokosoa utaratibu wa ripoti za kamati za bunge
kuwasilishwa serikalini kabla ya kufikishwa bungeni kama ilivyozoeleka, na kuwataka
wananchi kuwapuuza watu hao kwa kuwa hawana nia njema.
Akizungumza katika sherehe ya Makabidhiano ya taarifa za kamati maalum za kuchunguza
uvuvi wa bahari kuu na gesi asilia, Spika Ndugai amesema utaratibu huo ni mzuri
kwa kuwa unaweka mkazo katika utekelezaji wa ripoti hizo.
Spika Ndugai ameeleza kuwa “Sisi tumeanzisha utaratibu huu
ambako tunafanya kazi yetu tunakuja mbele ya umma tunawasilisha kazi yetu mbele
ya serikali yetu, eti tunaambiwa sisi tuna utaratibu mbaya, tuwapuuze watu wa
namna hii sababu hawana nia njema.”
“Ningependa kufafanua kitu kidogo, ziko namna mbalimbali ya
bunge kufanya kazi moja wapo ya ile tuliyoizoea ambapo bunge linafanya kazi
ndani ya ukumbi wa bunge, namna nyingine ndiyo hii ambapo spika akishauriwa na
kuona jambo hili lina msingi mkubwa anatumia mamlaka aliyonayo kufanya hivi
nilivyofanya. Na kwa mamlaka hayo hayo akaamua kuwasilisha ripoti ile kwa
serikali kwa utaratibu atakaona unafaa na utaratibu nilioona unafaa ni huu,”
amefafanua Spika Ndugai na kuongeza.
