Chama cha ACT-Wazalendo kimetoa ufafanuzi wa sintofahamu
kuhusu ushirikiano wake na Chadema katika kusimamisha mgombea mmoja kwenye
uchaguzi mdogo wa Jimbo la Buyungu unaotarajiwa kuitishwa baada ya mbunge wake,
Mwalimu Kasuku Bilago kufariki dunia.
Ufafanuzi huo umetolewa na Kiongozi wa Chama wa ACT, Zitto
Kabwe ambapo amesema uamuzi huo ni sehemu ya utekelezaji wa maazimio ya
mwelekeo wa chama hicho yaliyoafikiwa na kikao chake cha mwezi Januari mwaka
huu.
“Chama cha ACT Wazalendo Katika Kikao chake cha Januari
Mwaka 2018 kiliazimia katika mwelekeo wa Chama Mwaka 2018 kuwa ni Muhimu
kujenga mashirikiano na vyama vingine na makundi mengine ya kijamii. Mwelekeo
huo umewekwa hapa pia. Tunataka kujenga a DEMOCRATIC FRONT kwa kuhusisha wana
Demokrasia nchini kwa madhumuni ya kutetea, kuimarisha na kulinda demokrasia
yetu ya vyama vingi na kujenga Uchumi shirikishi wa Wananchi ( inclusive
economy),” amesema Zitto kupitia taarifa yake kwa umma aliyoitoa leo.
Zitto amefafanua kuwa “Mnamo tarehe 30/ 5/2018 Viongozi wa Vyama
2 vya upinzani nchini Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto na Freeman Aikael Mbowe
walitamka dhamira ya kushirikiana kwa kuanzia kuweka mgombea mmoja wa ubunge
Jimbo la Buyungu Mkoa wa Kigoma na hatimaye nchi nzima. Makubaliano haya ambayo
yanarejewa kama MAKUBALIANO YA KAKONKO hatimaye yatafikishwa kwenye vikao vya
Vyama vya ACT Wazalendo na CHADEMA ili kupata baraka za wanachama.”
