Mohammed Gulam Dewji ‘Mo’ Mmiliki wa hisi kubwa kwenye klabu ya Simba ameanzisha tuzo ndani ya klabu hiyo itakayotolewa kila msimu kwa wachezaji na viongozi na mashabiki wa klabu hiyo
Tuzo hiyo aliyoipa jina la Mo Simba Awards zitakazoanza kutolewa Juma tatu Juni 11 mwaka huu katika hoteli ya Hyatt Regency maarufu kama Kilimanjaro iliyopo mjini Dar es Salaam.
kupitia taarifa yake ‘Mo’ amesema kwamba tuzo hizo zitakuwa na vipengele 16, ambavyo ni Mchezaji Bora wa Mwaka, Goli Bora la Mwaka, Golikipa Bora wa Mwaka, Beki Bora wa Mwaka, Kiungo Bora wa Mwaka, Mshambuliaji Bora wa Mwaka, Shabiki Bora wa Mwaka na Tuzo ya Heshima.
Tuzo zingine ni Mchezaji Bora Mwanamke wa Mwaka, Mchezaji Bora Mdogo wa Mwaka, Tuzo ya Benchi la Ufundi, Kiongozi Bora wa Mwaka, Tuzo ya Wasimamizi wa Mchakato wa Mabadiliko, Mhamasishaji Bora wa Mwaka katika Mitandao ya Kijamii, Mhamasishaji Bora wa Mwaka na Tawi Bora la Mwaka.
Washindi wa tuzo hizo watatokana na kura ambazo zitapigwa na mashabiki kupitia mitandao ya kijamii na tovuti ya mosimbaawards.co.tz na kamati maalumu ya tuzo ambayo itahusisha wadau mbalimbali wa mchezo wa mpira wa miguu nchini.
Dewji amesema ameanzisha tuzo hizo kwa lengo la kutambua mchango wa wachezaji, viongozi na mashabiki ambao juhudi zao zimeiwezesha Simba SC kupata mafanikio iliyonayo sasa.
Dewji amesema tuzo hizo ni sehemu ya mikakati yake ya kuifanya klabu ya Simba kuwa timu kubwa barani Afrika, ambayo itakuwa na uwezo wa kifedha ambao utaiwezesha kuwa na wachezaji na benchi la ufundi bora ambalo litaiwezesha kushinda mataji makubwa.
“Simba ni timu kubwa inastahili kuwa na tuzo zake ambazo zitakuwa zinatolewa kwa kutambua mchango wa wenzetu ambao umetuwezesha kupata mafanikio haya ikiwepo kushinda taji la Ligi Kuu ya Tanzania Bara. Ni jambo ambalo litawatia moyo kuendelea kujituma lakini hata kwa ambao watakosa itawatia hamasa na hivyo kuongeza juhudi,” amesema Dewji.
