Serikali imetangaza mikakati yake minne katika kuboresha
matumizi ya gesi kwa wananchi, ikiwemo kuendeleza usambazaji wa mabomba ya gesi
majumbani, pamoja na kuanzisha mfumo wa wananchi kupatiwa mitungi iliyojaa gesi
bure, kisha kulipia gharama kadri wanavyotumia.
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Rais-Muungano na Mazingira, January Makamba katika sherehe ya ufunguzi wa wiki
ya misitu inayotarajiwa kuisha Juni 5, 2018 ambayo ni siku ya mazingira duniani,
iliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
iliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Waziri Makamba amesema serikali iko katika mazungumzo na
wauzaji wa mitungi ya gesi nchini ili waanzishe mfumo huo utakaosaidia wananchi
wengi hasa wa kipato cha chini kutumia nishati hiyo na kupunguza uharibifu wa
mazingira.
“Matumaini mengine ni gesi ya mitungi, mimi nimekuwa mlezi
wa wauzaji wa gesi tumewaomba waunde chama ili waweze kuleta mambo yao serikalini
ili kusaidia bei ya uuzaji mitungi ya gesi ishuke gharama. Kuna ubunifu katika
eneo hili,” amesema Waziri Makamba na
kuongeza.
“Moja ya sababu iliyokuwa inasababisha watu wasitumie
mitungi ni gharama ya mitungi, lakini sasa hivi kuna kampuni inajaribisha
teknolojia na sisi tumewahimiza, ubunifu sababu sasa itawezekana katika mtungi
ule wa laki moja kuna mita ambapo unaweza kuingiza kwa kutumia M-pesa kununua
gesi, atapewa mtungi umejaa gesi lakini analipa fedha kwa kadri anavyotumia kwa
M-pesa katika mita aliyolipa pale.”
