Ikiwa imepita siku moja tangu
Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe kulilalamikia bunge kwamba halikuwa
mstari wa mbele katika kumuuguza aliyekuwa Mbunge wa Buyungu, marehemu Kasuku
Bilago, Spika Job Ndugai amevunja ukimya kuhusu malalamiko hayo.
Spika Ndugai amemjibu Mbowe akisema
kuwa, kama anataka uthibitisho kuhusu bunge lilivyojitolea kuhudumia matibabu
ya marehemu Bilago, amuulize mke wa marehemu.
Amesema bunge lilimtunza marehemu
Bilago na kumlipia gharama za matibabu tangu alipolazwa jijini Dodoma, pamoja
na kukodisha ndege kwa ajili ya kumsafirisha kutoka Dodoma hadi Dar es Salaam
na kumfikisha katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako umauti ulimfika wakati
akipatiwa matibabu.
“Mumtafute mke wake, ndio anaweza
kuwaeleza kuhusu Bunge, ambao ndio tumemtunza tangu anaugua na kulipa gharama
zote za matibabu, mpaka amefariki mikononi mwetu tukiwa tunamtunza mgonjwa,
ukishafanya yote hayo halafu mtu aliyekuwepo nje ya nchi, anasema kwamba wewe hakuna
ulichokifanya, tuseme tu Haleluya Inatosha,” alisema Ndugai.
