ACT yajuta kumtwika zigo la korosho Waziri Tizeba


Chama cha ACT Wazalendo kimesema kilifanya makosa kumtaka Waziri wa Kilimo, Dkt. Charles Tizeba kujiuzulu kutokana na kuzorota kwa sekta ya korosho nchini kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo upungufu wa pembejeo ya zao hilo.

Akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi na Uenezi ACT, Ado Shaibu amesema mwanzo chama hicho kilidhani Dkt. Tizeba ndiyo sababu ya kuzorota kwa sekta hiyo  kwa kushindwa kupeleka pembejeo kwa wakulima, lakini sasa imebaini kwamba ucheleweshaji wa serikali katika kutoa fedha za mauzo ya nje za korosho ghafi ndiyo sababu ya kudorola kwa sekta hiyo.

Ado amesema kuwa, serikali imeshindwa kutoa fedha za mauzo hayo kiasi cha Sh. Bilioni 211 katika kipindi cha miaka miwili kuanzia mwaka wa fedha wa 2016/17 na 2017/18 kwa Mfuko wa Bodi ya Korosho kwa ajili ya kugharamia uendeshaji wa zao hilo.


 “Kwa mujibu wa taarifa ya bodi ya korosho iliyotolewa na Kamati ya Bunge ya Maji, Umwagiliaji, Kilimo na Mifugo, kwa msimu wa mauzo ya korosho wa 2016/17 yaliyokuwa bilioni 91, na 2017/18 yalikuwa 110, bodi ilikuwa haijapokea jumla ya Sh. Bilioni 211,” amesema Ado. 

Post a Comment

Previous Post Next Post