Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe ameeleza kusikitishwa kwake na ratiba ya mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Buyungu, Kasuku Bilago iliyotolewa na Bunge siku mbili zilizopita, akisema kuwa maamuzi hayo hayakushirikisha chama hicho na familia ya marehemu.
Bunge kupitia ofisi ya katibu mkuu ilitoa ratiba ya mazishi ya marehemu
Bilago, ambapo ilipanga mwili wake uagwe bungeni leo Jumatatu, lakini Mbowe
amesema hatua hiyo imewahuzunisha sana kutokana kwamba imelenga kuharakisha
mazishi ya Bilago.
“Bunge limeundwa na sehemu kuu mbili, serikali na kambi ya
upinzani, katika kambi ya upinzani tuna vyama vingi, na upande wa serikali una
ccm.bSisi tunaelewana sana lakini upande wa pili kuna urafiki wa mashaka na
popote wanapojipa jukumu la kufanya maamuzi kuhusu upande wetu yamekuwa hayana
nia njema,” amesema na kuongeza.
“Bilago alifariki jumamosi mchana, saa kumi jioni ofisi ya
bunge imetangaza taratibu za mazishi wakati tuko katika harakati za kuhifadhi
mwili, hatujakaa kikao, hatujawasiliana na ndugu, huyu ni kiongozi wa mikoa
mitatu na mbunge. Pasipo mazungumzo ofisi inatoa taarifa ya mazishi hilo jambo
limetuhuzunisha sana. Wamesema bilago aagwe leo kama wangekuwa wanampenda
wamemtibu kwanza.”
Mbowe ameongeza kuwa “Wanataka kuharakisha kumzika kiongozi
wetu, nikamwambia spika hatutokuja Dodoma Jumatatu. Ngoja tufanye mawasiliano
na familia, familia ikasema Alhamisi ndiyo siku nzuri ya mazishi, sisi kama
chama tulikubaliana na familia tukaiarifu ofisi ya bunge kwamba tutamlaza
Alhamisi kijijini kwao, tukapanga ratiba asubuhi atapelekwa Dodoma kwa ajili ya
wabunge wenzake kisha atapelekwa kigoma kwa ndege.”
