Baada ya kukabidhiwa rasmi ofisi,
Katibu Mkuu mpya wa CCM, Dkt. Bashiru Ally amesema kazi aliyopewa na
Halmashauri kuu ya chama hicho ni kufanya siasa ya mezani na si ya majukwaani,
na kwamba atazungumzia na au kuchambua masuala yanayoamuliwa na kamati hiyo.
Dkt. Bashiru amesema maneno hayo
mbele ya wanahabari baada ya kukamilika kwa shughuli ya makabidhiano ya ofisi iliyofanyika
leo Mei 31, 2018 katika ofisi ndogo ya CCM iliyoko Lumumba jijini Dar es
Salaam. Amekabidhiwa ofisi na Abdulrahman Kinana aliyejiuzulu wadhifa huo.
“Kazi niliyopewa si ya jukwaa, si siasa ya majukwaani, siasa
ya majukwani ni ya mwenyekiti wa chama
akisaidiwa na makamu wake wawili, kule mikoani tuna wenyeviti wa vyama, wabunge
na madiwani. Nazungumza kama katibu mkuu nikiwa msemaji wa chama na msimamo wa
vikao vya halmashauri kuu ambacho ndio chombo kilichoniteua na chenye uwezo wa
kunifukuza, siwezi kuchambua yale yasiyoamuliwa kwenye kikao,” amesema Dkt.
Bashiru.
Dkt. Bashiru ameongeza kuwa “Ni marufuku kwa watendaji
kufanya kazi ya wanasiasa, kazi ya kupiga siasa safi ni ya wale waliochaguliwa
kwa muda wa miaka mitano, kama mtendaji hamtaniona kwenye majukwaa sababu wapo
waliopewa dhamana ya kusema kwenye majukwaa, kazi yangu mimi ni kutoa taarifa
kwenye vikao, kusimamaia maelekezo ya chama hayo si masuala ya jukwaani masuala
ya mezani.”
