Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Dk Wilbrod Slaa amewapa wapinzani
nchini, mbinu za jinsi ya kukabiliana na changamoto za kisiasa zinazowakabili,
badala ya kulalamika.
Kadhalika,
Dk Slaa, ambaye alikuwa katibu mkuu wa Chadema, amesema kabla vyama hivyo vya
upinzani kulalamika, vinapaswa kutumia sheria kupata haki zao kama yeye
alivyofanya mwaka 2011.
Akizungumza
kwa njia ya simu katika mahojiano maalumu na gazeti hili jana, Dk Slaa ambaye
alitangaza kuachana na siasa za vyama muda mfupi kabla ya Uchaguzi Mkuu wa
mwaka 2015, alisema badala ya wapinzani kulalamika wanaweza kutumia sheria
zilizopo ili kupata haki ya jambo lolote ambalo wanahisi wanaonewa au haliendi
sawa.
Kwa
muda mrefu vyama vya upinzani vimekuwa vikitoa malalamiko yao kwamba vinaminywa
na kutopatiwa haki huku wakitoa mifano ya kuzuiwa kufanya mikutano ya hadhara
na kunyimwa haki ya kuandamana.
“Wamelalalamika
kwa muda mrefu na mara kadhaa nimekuwa nikishauri hili. Narudia, tutafakari. Si
muda wa kulalamika tena sasa ni kuchukua hatua,” alisema Dk Slaa aliyewahi kuwa
mbunge wa Karatu kwa tiketi ya Chadema.
“Nionyesheni
ni wapi sheria au kanuni yoyote inakataza kufanya mikutano au maandamano?
Nionyesheni ni wapi tamko la Rais linaweza kufuta sheria zilizopo? Mimi ni
mwanasheria, najua maana ya sheria. Hayo yote ni matamko tu. Rais hawezi kufuta
sheria kwa tamko.”
Dk
Slaa alisema wapinzani wanachotakiwa kufanya kwa sasa ni kutumia sheria
kuhakikisha wanapata haki zao kama wanaamini kuwa zinaminywa.
“Wanaweza
kutumia sheria ya The Basic Right and Judgment (Sheria ya Haki za Msingi na
Hukumu) ya mwaka 1994 kufungua kesi mahakamani wamshtaki Rais au kiongozi
yeyote ambaye wanaamini hawatendei haki, kuacha kufanya hivyo,” alisema.
“Lengo
la sheria hii ni kuhakikisha inatoa haki kwa yeyote au kiongozi yeyote, akiwamo
Rais ambaye anaonekana ama hatendi au kuminya kwa haki zake za msingi, unapaswa
kwenda mahakamani na kutafsiri sheria hiyo.”
Dk
Slaa alisema si vizuri wanasiasa wakalalamika tu bila kuchukua hatua wakati
sheria zipo.
Dk
Slaa alisema wakati akiwa mbunge, alikuwa akibughudhiwa na Jeshi la Polisi mara
kwa mara, akikamatwa na kufikishwa mahamani bila sababu za msingi, lakini
alipogundua kuwa anaweza kwenda mahakamani kuomba tafsiri hiyo, alichukua
hatua.
“Mwaka
2011 nilitumia sheria hiyo, nikafungua kesi mahakamani. Chini ya sheria hii
kesi inabidi kusikilizwa chini ya majaji watatu na mwaka 2013 nilishinda. Toka
pale sikushtakiwa tena,” alisema.
Alitoa
mfano mwingine wa mwaka 2002 wakati akiwa mbunge wa Karatu. alisema wakati huo
Rais aliyekuwapo alitaka kuifuta Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, lakini yeye
(Dk Slaa) alishirikiana na madiwani kufungua kesi ya kupinga isifutwe, jambo
lililompa hofu hata jaji aliyekuwapo.
“Tulifungua
kesi dhidi ya Rais aliyekuwapo, lakini baadaye kesi ile ilifutwa kwa kuwa
ilionekana tunawaaibisha. Mimi si mtu wa kulalamika, nawasihi hata wao
wasilalamike wafuate njia sahihi,” alisema.
Katibu
huyo mkuu wa zamani wa Chadema aliwashangaa viongozi wa upinzani kuacha haki
yao ikandamizwe ilhali walishawahi kwenda mahakamani mara kadhaa katika kesi
mbalimbali na nyingi ziliisha kwa wao kushinda.
“Kinachonishangaza
na sina jibu mpaka sasa kwa nini hili linawashinda sasa, hasa ukizingatia hivi
sasa vyama vina mawakili na wapenzi wengi tofauti na ilivyokuwa awali? Mimi
nilishinda kipindi ambacho hakuna mawakili wengi, kwa nini wao wanaendelea
kulalamika?
“Kama
kweli wana nia ya dhati ya kutaka Rais au kiongozi yeyote asiendelee
kuwabughudhi, wachukue hatua mapema.”
Dk
Slaa alisema siasa peke yake yake haisaidii na badala yake lazima ifanywe kwa
misingi ya sheria ingawa alikubali kuwa kuna sheria nyingi nzuri ambazo
hazisimamiwi.
Hata hivyo, alisema kinachotokea sasa ni nguvu aliyonayo Rais John
Magufuli katika kutekeleza mambo mbalimbali, kama sheria ambazo awali zilikuwa
hazitekelezwi.
“Tulikuwa na viongozi dhaifu lakini sasa Rais Magufuli amekuja, ameamua
kusimamia sheria zote ndiyo tunalalamika. Mfano kulikuwa na Sheria ya Polisi,
lakini ilikuwa haitekelezwi. Sasa amepatkana mwenye kauli inatekelezwa, lakini
watu wanalalamika,” alisema.
Madai ya usaliti
Dk Slaa, ambaye aliondoka Chadema katika kipindi muhimu cha kuelekea
Uchaguzi Mkuu, anasema uamuzi wake si usaliti na kwamba tuhuma dhidi yake
hazina mashiko.
“Mengi yamesemwa, lakini nikwambie tu huo ni upotoshaji mkubwa na kwamba
mimi hilo halinisumbui. Ningeumia endapo kama kitu kinachozungumzwa kina
ukweli,” alisema.
Alisema yeye ni “yuleyule na atabaki kuwa yuleyule” ambaye hoja yake ni
mapambano dhidi ya ufisadi na hatanyamaza katika hilo.
Alisisitiza kuwa, kutokana na tuhuma hizo, aliamua kuandika kitabu
ambacho kilikamilika February 2017 na sasa kiko katika hatua za mwisho za
uchapishaji kabla ya kukizindua rasmi.
Dk Slaa alisema kitabu hicho kitakuwa na majibu yote ikiwamo tuhuma za
usaliti.
“Watanzania wajiulize wako wapi sasa wale waliobadili gia angani,
niwaambie tu Dk Slaa wa mwaka 1995 aliyekuwa akipinga ufisadi mpaka 2015
alipoachana na siasa vya vyama ni yuleyule, sijawahi kubadilika wala kuwa
msaliti,” alisema.
“Hao wanaosema mimi msaliti waniletee ushahidi na nakwambia kama kuna
yeyote ambaye atafanikisha kuleta hata nukta, nipo tayari kula matapishi
yangu.”
Dk Slaa, ambaye baada ya kuachana na siasa aliamua kwenda kuishi nchini Canada,
aliwashangaa wanaohusisha kukubali uteuzi wa kuwa balozi na usaliti.
Alisema wanaohusisha vitu hivyo viwili hawajui majukumu ya balozi kwa
kuwa hayana uhusiano na siasa.
Alisema yeye kama balozi ni kweli yupo serikalini, lakini majukumu yake
ni tofauti na viongozi wengine wa Serikali.
“Balozi ni mwakilishi wa Rais kwa mkuu wa nchi nyingine, pale unakwenda
kwa ajili ya masilahi ya Taifa, hivyo siendi pale kwa ajili ya kuiwakilisha CCM
au Chadema,” alisema.
Alisema anachosimamia kwa sasa ni sera ya nchi ambayo ilipitishwa wakati
yeye akiwa mbunge na kuwa hata Rais Magufuli anatekeleza kitu ambacho
kilishapitishwa wakati huo na ambacho hakikutekelezwa.
Alisema wajibu wake ni kudumisha na kukuza uchumi na siasa baina ya nchi
hizo mbili.
Mwanasiasa huyo alisema wakati wote akiwa mbunge alikuwa akifanya kazi za
kitaifa na ndiyo sababu katika uongozi wake hakuwahi kusikika akiomba fedha za
ujenzi wa miundombinu kama barabara, maji au zahanati.
Alisema badala yake alifanya kazi za kitaifa na kuomba fedha za maendeleo
ya jimbo lake kutoka kwa wafadhili.
“Tangu 1995 nilipeleka maendeleo jimboni kwangu bila kutegemea fedha za
Serikali, sasa leo itanishinda nini kwa wadhifa nilionao kutafuta watalii waje
nyumbani ili tukuze uchumi, kutafuta wawekezaji ili kuwekeza na kuongeza ajira
ili pato letu liongezeke,” alisema.
“Sijaanza leo kazi hii, nilianza Karatu na matunda yangu yanaonekana
ndiyo maana leo Karatu ni tofauti na majimbo mengine.”
Chanzo: Mwananchi