Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi-CUF, Maalim Seif Shariff
Hamad amemwandikia barua Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi
kuhusu mkutano mkuu wa chama hicho
uliotishwa na Mwenyekiti wake anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vyama
vya siasa, Profesa Ibrahim Lipumba.
Taarifa hiyo imetolewa asubuhi ya leo kwa umma na Naibu
Mkurugenzi wa Habari, Mawasiliano na Umma, Mbarala Maharagande.
Sehemu ya taarifa hiyo inaeleza kuwa, mkutano huo
unatarajiwa kufanyika Juni 17, 2018 mkoani Singida ambapo Jaji Mutungi
anatarajiwa kuhudhuria katika mkutano huo. Barua ya Maalim Seif iko hapo chini.
THE CIVIC UNITED FRONT (CUF- Chama Cha Wananchi)
Office of the Secretary General, Party Headquarters, P.O. Box 3637, Zanzibar, Tanzania
Our Ref:
CUF/HQ/AKM/003/018/09 Date: 21 Mei, 2018
Mhe. Jaji Francis
Mutungi
Msajili wa Vyama vya Siasa
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa
Kivukoni Ilala CBD
1 Shaaban Robert Street
P.O. Box 63010
DAR ES SALAAM
KUH: KUENDELEA KUTUMIA VIBAYA DHAMANA ZAKO NA OFISI
UNAYOIONGOZA KUENDESHA NJAMA ZA HUJUMA DHIDI YA THE CIVIC UNITED FRONT (CUF –
CHAMA CHA WANANCHI)
Tafadhali husika na mada iliopo hapo juu.
THE CIVIC UNITED FRONT (CUF – Chama Cha Wananchi) ambacho ni
chama cha siasa halali ndani ya Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania, kimepata
taarifa za uhakika kwamba katika kuendeleza njama zako ovu dhidi ya chama chetu
na ili kuvuruga mwenendo wa kesi zinazoendelea katika Mahakama Kuu ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania kuhusiana na mambo kadhaa yanayokihusu chama chetu na
ambayo pia yanakuhusisha wewe na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa
unayoiongoza, umemuelekeza Ibrahim Haruna Lipumba na genge lake waandae Mkutano
Mkuu batili wa Taifa (fake National Conference) hapo tarehe 17 Juni, 2018 kwa
madhumuni ya kuwaondoa viongozi halali waliopo wa Chama na nafasi zao kuwaweka
viongozi batili.
Taarifa hizo za uhakika tulizozipokea zinasema kwamba
umewaelekeza kwa sababu za kimkakati Mkutano Mkuu huo batili uwe wa kushtukiza na
usifanywe Dar es Salaam wala Zanzibar na badala yake wafikirie Singida, Mwanza,
Tabora au Morogoro.
Kwa malengo ya kufanikisha njama hizo chafu na za kihuni,
taarifa zimetuthibitishia kwamba wewe kupitia mwendelezo wa kuitumia kwako
vibaya dhamana uliyopewa na pia kuitumia vibaya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya
Siasa, umewahakikishia kwamba utawapatia ‘mkopo’ wa shilingi milioni 600/-
mwisho wa mwezi huu wa Mei, na kwamba tarehe 15 Juni fedha hizo zitaachiwa
kwenda akaunti ya Temeke (ambayo ndiyo mmekuwa mkiitumia kufanyia uhalifu wa
kuhamisha fedha za ruzuku ya CUF kuwapa Lipumba na genge lake kinyume na
sheria) na zitachukuliwa zote kwa pamoja kama fedha taslimu (cash) kwenda
sehemu itakayoamuliwa kufanyia Mkutano Mkuu huo batili.
Tunazo taarifa kwamba katika maelekezo yako hayo uliyowapa
Lipumba na genge lake umewaambia wasishughulike na masharti na matakwa ya
Katiba ya THE CIVIC UNITED FRONT (CUF – Chama Cha Wananchi) ya mwaka 1992
(Toleo la 2014) katika kufanya Mkutano Mkuu huo batili kwani wewe utautambua na
kuidhinisha maamuzi yake.
Kwa kuwa wewe ndiye mwenye kuhifadhi katiba za vyama vyote
vya siasa, nina hakika unajua kwamba kipindi cha uongozi wa Chama ndani ya CUF
ni miaka mitano. Ibara ya 113 ya Katiba ya CUF ya 1992 (Toleo la 2014)
inaeleza:
“113. Isipokuwa pale ambapo Katiba imeeleza vinginevyo
masharti ya kuchaguliwa kwa kiongozi
na kipindi cha uongozi kitakuwa kama hivi:-
(1) Kipindi
cha uongozi wa Chama kitakuwa miaka mitano (5) kwa ngazi zote isipokuwa kama
kiongozi huyo ameshindwa kazi aliyopewa.
(2) Iwapo
kipindi cha uongozi kimemalizika na kuna sababu za msingi na za kitaifa
kusababisha kwamba uchaguzi wa viongozi hao hauwezi kufanyika basi muda wa
uongozi utaendelea kwa kipindi kingine cha miezi isiyozidi sita (6) na baada ya
hapo ni lazima uchaguzi mpya uitishwe.”
Uongozi wa Chama uliopo ulichaguliwa kupitia Mkutano Mkuu wa
Taifa uliofanyika mwezi Juni, 2014 na ambao taarifa za kumbukumbu zake zote
unazo kwani ziliwasilishwa kwako rasmi kama Sheria ya Vyama vya Siasa
inavyoelekeza. Ndiyo kusema kipindi cha uongozi uliopo kinamalizika Juni 2019.
Kutaka kwako kulazimisha uchaguzi batili na haramu kupitia Lipumba na genge
lake kipindi hiki ni kukiuka masharti ya Katiba ya CUF ambayo wewe ukiwa mwenye
dhamana ya kutunza Katiba za Vyama unapaswa kuilinda na kuitetea.
Isitoshe kutokana na kesi zilizopo Mahakamani ambazo
zinahusu kupata uhalali wa vyombo muhimu vya Chama na maamuzi yake, hiyo
inatosha, ikiwa patakuwa na haja hiyo, kuwa sababu iliyoelezwa katika Ibara ya
113(2) tuliyoinukuu hapo juu ya kusogeza mbele Uchaguzi wa Chama ndani ya Chama
kwa kipindi kisichozidi miezi sita (6).
Mbali ya hayo, kwa mujibu wa Ibara ya 63(2)(iv) na (v), na
Ibara ya 78(1)(l) na (m), utaratibu wa kuwapata wajumbe wa Mkutano Mkuu wa
Taifa wakati wake ukifika unaujua kwamba ni kupitia uchaguzi unaofanywa na
ngazi ya uwakilishi ambayo ni Mikutano Mikuu ya Wilaya za Tanzania Bara na
Zanzibar. Wajumbe wengine wa Mkutano Mkuu wa Taifa wanatajwa katika Ibara ya
78(1)(a) –(t). Wajumbe wa Mikutano Mikuu ya Wilaya nao wanatokana na Kata kwa
Tanzania Bara na Majimbo kwa Zanzibar [Ibara ya 62(2)(a)-(p)] ambapo Wajumbe wa
Mikutano Mikuu ya Kata [Ibara ya 31(2)(a)-(h)] na Majimbo [Ibara ya
45(2)(a)-(h)] nao wanatokana na Mikutano Mikuu ya Matawi inayowajumuisha
wanachama wote waliomo kwenye matawi husika [Ibara ya 17(2)].
Masharti haya ya Katiba ya CUF ya 1992 (Toleo la 2014)
unayafahamu vyema maana yamekuwa yakisimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya
Siasa kwa miaka yote kabla ya wewe kukubali kujishusha hadhi na kutumika
kuyavuruga kwa maslahi yako na wale unaowatumikia.
Tunajua kuwa makubaliano yenu (kati yako na Lipumba na genge
lake) kulingana na maelekezo yako ni kwamba genge hilo waonekane tu wamesambaza
fomu za uchaguzi wa Chama ndani ya Chama hata bila ya kuzingatia na kufuata
maelekezo na masharti ya Katiba ya Chama na Kanuni za Uchaguzi wa Chama ndani
ya Chama. Umewaelekeza kuwapa watu wowote, hata kama si wanachama wa CUF, fomu
hizo ili wazijaze na kisha kuwapanga katika nafasi mbali mbali za uongozi wa
ndani ya Chama ikiwemo ujumbe batili wa Mkutano Mkuu huo batili (ambalo ndilo
lengo kuu) hata kama hakutafanyika uchaguzi.
Maelekezo hayo umewapa baada ya kushindwa kwenu na njama
zenu za awali za kuwarubuni viongozi wa Chama halali na wajumbe halali wa
Mkutano Mkuu wa Taifa kutoka kwenye Wilaya za Tanzania Bara na Zanzibar ili
wafanye kile mnachokitaka ambapo viongozi na wajumbe hao halali walikataa
kutumika kukivuruga na kukihujumu chama chao wenyewe walichokijenga kwa jasho
lao na damu zao kupitia mateso makubwa waliyopitishwa na dola tokea 1992 hadi
hii leo.
Katika njama zenu hizo chafu na za kihuni, umewahakikishia
Lipumba na genge lake kwamba wakifanikisha maelekezo uliyowapa, wewe utautambua
uongozi batili utakaopachikwa na baada ya hapo vyombo vya dola vitakamilisha
kazi iliyobaki ya kuzidhibiti ofisi zote za CUF nchi nzima na kuzikabidhi kwa
Lipumba na genge lake. Umewaambia baada ya hapo, hata viongozi halali wa Chama
tukifungua kesi kupinga uhuni huo mnaouandaa itachukua mwaka mwingine mzima na
hivyo kufanikisha malengo yenu maovu.
Hivi ndivyo mtu mwenye nafasi ya Jaji wa Mahakama Kuu
ulivyoamua kujidhalilisha alimradi tu unafanikisha matakwa yako binafsi na ya
wale waliokutuma, lengo likiwa ni kuviua vyama makini vya siasa vinavyotoa
ushindani wa kweli dhidi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Imeamuliwa kuihujumu CUF
mara tu baada ya kile kilichoitwa uchaguzi wa marudio Zanzibar kutokana na CUF
kuishinda vibaya CCM katika nafasi ya Urais wa Zanzibar, Ujumbe wa Baraza la
Wawakilishi na Madiwani katika uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa tarehe 25 Oktoba,
2015. Imeamuliwa pia kuihujumu CUF kwa sababu ya kuwa mshirika muhimu ndani ya
Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ambao uliipa wakati mgumu CCM katika
uchaguzi mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa tarehe 25 Oktoba, 2015
kuliko wakati mwengine wowote tokea ulipoanzishwa tena mfumo wa vyama vingi vya
siasa mwaka 1992. Lengo ni kuwa na CUF kama chama kibaraka (puppet party)
kitakachoongozwa na vibaraka wa CCM ili kukisaidia watawala hao wabaki
mdarakani.
Najua hii si mara ya kwanza kukuandikia na kukueleza kuhusu
ushiriki wako binafsi na wa ofisi ya umma unayoiongoza, Ofisi ya Msajili wa
Vyama vya Siasa, katika kupanga,
kuendesha na kuongoza hujuma dhidi ya chama chetu, THE CIVIC UNITED FRONT (CUF
– Chama Cha Wananchi). Sitowacha kufanya hivi nikitambua kama unavyotambua wewe
kwamba kufanya hivi ni kuweka kumbukumbu za haya unayotenda. Kwa upande wetu
sisi tutahakikisha tunakilinda Chama chetu na tunailinda demokrasia ndani ya
nchi yetu na tunaulinda mfumo wa vyama vingi vya siasa hapa nchini.
HAKI SAWA KWA WOTE
SEIF SHARIF HAMAD
KATIBU MKUU
Nakala kwa:
§ Mhe. Jenesta
Mhagama (MB),
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu,
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
DODOMA.
§ Mhe. Jaji Mkuu,
Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
DAR ES SALAAM.
§ Mhe. Jaji Kiongozi,
Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
DAR ES SALAAM.
§ Mkuu wa Jeshi la
Polisi (IGP),
Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania,
DAR ES SALAAM.
