Chama cha ACT-Wazalendo kimetoa salamu za pole kwa chama cha
Chadema, bunge na familia ya aliyekuwa Mbunge wa Buyungu mkoani Kigoma, Kasuku
Bilago aliyefariki jana katika hospitali ya taifa Muhimbili.
Salamu hizo zimetolewa leo Mei 27, 2018 na Katibu wa Itikadi
na Uenezi ACT, Ado Shaibu wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar
es Salaam.
Ado amesema ACT itashirikiana kwa karibu na familia ya
marehemu ya Bilago katika kufanikisha shughuli za mazishi.
“ACT tunapenda kutoa pole kwa Chadema, bunge na wananchi wa
Buyungu mkoani Kigoma kwa kuondokewa na mbunge wao mpendwa Kasuku Bilago, katika
kipindi hiki kigumu tuko nao bega kwa bega,” amesema Ado.
Taarifa ya ofisi ya bunge iliyotolewa jana kwa umma,
ilieleza kuwa mwili wa marehemu Bilego unatarajiwa kuagwa kesho bungeni jijini
Dodoma kisha kusafirishwa Kankonko mkoani Kigoma kwa ajili ya mazishi.
