Kampuni ya Terranova imeandaa maonyesho ya milki kuu , nyumba na nyenzo za ujenzi katika viwanja vya bunge Dodoma.
Maonyesho hayo yamezinduliwa rasmi leo na waziri wa ardhi William Lukuvi ambapo wadau mbalimbali wamejitokeza kuonyesha bidhaa mbalimbali katika sekta hiyo wakiwemo, Nabaki Afrika, Fumba developments, Ngorongoro conservativation, Alrais developers na taasisi ya mwanamke ardhi.
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Terranova, Emil Sylvester amesema kuwa kampuni hiyo imeanza kuhamasisha wawekezaji wafike Dodoma ili kufanikisha adhma ya serikali ya kuhamia mjini humo.
"Sisi tumeanza na tutazidi kuhamasisha wawekezaji wafike Dodoma , ili adhma kuu ya serikali ya kuhamia Makao makuu ya nchi izidi kupata tija kwa maendeleo yetu," amesema Sylvester.
Hata hivyo Waziri Lukuvi amesema kuwa pamoja na ubunifu huo wa waandaaji uliolenga kuwafikia watanzania wote kwa wakati mfupi kupitia wawakilishi wao, itasaidia kufikisha elimu kuhusiana na sekta nzima ya ardhi na kuiletea Tanzania mendeleo makubwa kutokana na rasilimali hiyo.
Lukuvi ameupongeza uongozi wa Kampuni ya hiyo inayoongozwa na vijana waliopata elimu katika vyuo vikuu hapa nchini na kutoa rai kwa wadau kulipa kodi halali katika uendeshaji wa shughili zao ili kwenda sawa na kasi ya ukuaji kiuchumi kupitia mapato ya ndani.


