Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) leo Aprili 17, 2018 iko katika hatua za kukamilisha upelelezi wa tuhuma za ubadhirifu wa zaidi ya Sh. 2 bilioni zinazowakabili viongozi wa kiwanda cha kukoboa Kahawa mkoani Kilimanjaro.
Viongozi kadhaa wa kiwanda hicho kinachomilikiwa na Vyama vya Ushirika katika Kanda ya Kaskazini wanatuhumiwa kuuza nyumba za ushirika kisha kununua mtambo feki wa kukoboa Kahawa ambao haujafanya kazi tangu ununuliwe miaka minne sasa.
Kaimu Kamanda wa TAKUKURU mkoani Kilimanjaro, Moses Oguda amesema kuwa baadhi ya majalada ya kesi hiyo yamerejeshwa kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini kwa ajili ya utekelezaji.
TAKUKURU pia imepokea taarifa za rushwa zipatazo 15 na kuzifanyia kazi, nyingi kati ya hizo zikiwa ni kutoka idara za Elimu, Serikali za Mitaa, Polisi na Mahakama.
