Burundi kuitangaza katiba mpya Alhamisi, nchi za kigeni, muungano wa Ulaya zachachamaa


Nchi ya Burundi inatarajia kuitambulisha Katiba mpya siku ya Alhamisi, ambapo taarifa ya Ikulu imethibitisha kwamba sherehe za utiaji sahihi kwenye katiba hiyo zitafanyika katika mkoa wa Gitega.
Aidhaa taarifa hiyo ya Ikulu imetoa mwaliko kwa magavana wote na Wakuu wa tarafa za Burundi kushiriki kwenye sherehe hizo. Wamealikwa pia wawakilishi wa vyama vya kisiasa , asasi za kiraia pamoja na Viongozi wa kidini .
Itakuwa mara ya kwanza katika historia ya Burundi kuwa na sherehe za kuipokea katiba mpya. Wadadisi wa siasa za Burundi wanahisi utaratibu huo mpya ni ujumbe wa Rais Pierre Nkurunziza wa azama yake ya kukamilisha shughuli ya katiba ambayo yeye ameipigia debe kwamba inakuja kuipa Burundi hadhi na Uhuru wake kamili wa kujitawala .
Hata hivyo wapinzani na baadhi ya nchi za kigeni wamekosoa mchakato huo mzima kwamba haukuzingatia sheria na katiba mpya inanuwia kumbakiza madarakani Rais Pierre Nkurunziza hadi mwaka 2034.

                       
Vile vile, Wajumbe wa Muungano wa Ulaya wamelichagiza Shirika la Muungano wa Afrika kuchukua mikononi mazungumzo ya amani ya Burundi kwa madai kwamba Jumuiya ya kimataifa imeanza kupoteza imani kwa mchakato wa upatanishi unaosimamiwa na Jumuiya ya Afrika ya mashjariki na inayoongozwa na Rais Museveni pamoja na msuluhishi Benjamin Mkapa.

Chanzo: BBC Swahili

Post a Comment

Previous Post Next Post