Nchi za Afrika Mashariki hivi karibuni zimechachamaa kufanya
mabadiliko na kutekeleza sheria za mtandaoni, huku sababu kuu ya msukumo huo
ikiwa ni kudhibiti uhalifu wa mtandaoni ikiwemo usambazaji wa taarifa za uongo
na uchochezi.
Leo Juni 1, 2018 nchi ya Rwanda imeungana na nchi nyingine
za ukanda huo kufanya maboresho ya sheria za mtandaoni ambapo bunge lake
lilipitisha sheria ya uhalifu wa mtandaoni yenye nia ya kusaidia sekta za
kiserikali na binafsi kudhibiti uhalifu huo kwa kulinda taarifa za serikali na
binafsi.
Hatua hiyo ya Rwanda pia ilifanywa na Uganda ambapo Rais
wake Yoweri Museven hivi karibuni alipendekeza Waganda wanaotumia mitandao ya
kijamii hasa wa Facebook na WhatsApp watozwe kodi ili kukabiliana na tatizo la usambazaji
habari za uongo, lakini mapendekezo hayo yamesitishwa baada ya wizara ya fedha
nchini humo kutaka kushauriana na wadau kuhusu uidhinishwaji wa mpango huo.
Nchini Kenya, Rais Uhuru Kenyatta hivi karibuni aliidhinisha
mswada wa uhalifu wa kompyuta na mtandaoni wa 2018 kuwa sheria. Ambapo sheria
hiyo itatoa adhabu ya Sh. Milioni 5 au kifungo cha miaka miwili jela na au
adhabu zote mbili kwa atakayepatikana na kosa la usambazaji wa taarifa za
uongo.
Wakati hayo yakijiri Kenya, Uganda na Rwanda, kwa upande wa
Tanzania kuna sheria ya makosa ya mtandaoni ya mwaka 2015 ambayo inatumika kwa
ajili ya kudhibiti vitendo vya uhalifu mtandaoni.
