Mwanzilishi wa mtandao wa
JamiiForums, Maxence Melo na mwenzake Micke William wameachiwa huru na Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kukutwa hawana kesi ya kujibu katika Kesi namba
457 iliyokuwa ikiwakabili iliyofunguliwa na Jamhuri kuhusu kampuni ya CUSNA
Investment iliyodaiwa kufoji nyaraka bandarini, kukwepa kodi na kuwatesa
wafanyakazi wazalendo na kupendelea wageni toka nje ya nchi.
Akisoma shauri hilo Hakimu
Godfrey Mwambapa amesema Washitakiwa hawana kesi ya kujibu na hiyo Mahakama
imewaachia huru kuanzia leo.
Katika kesi hiyo, Polisi walitaka
JamiiForums iwapatie taarifa za mwanzisha mada aliyefahamika kwa jina la Kwayu
na mchangiaji mmoja Amri Shipuri ili waweze kuwakamata na kuwahoji kutokana na
ukiukwaji wa taratibu.
JamiiForums inadaiwa kuwa,
ilikataa kutoa taarifa binafsi za mwanachama wake kwa kuamini kuwa chanzo hcho
cha taarifa kilikuwa na nia njema hivyo kutaka kwanza iwepo Hati ya Mahakama
inayoridhia kukamatwa kwa mhusika na kuelezwa kosa lake.
Kesi hiyo ni kati ya mashauri 3
yaliyokuwa yanawakabili washtakiwa, na kwamba kwa sasa bado kuna mashtaka 2
yanayowakabili washtakiwa hao, yatakayotajwa mahakamani hapo Juni 18 mwaka huu.
