Serikali imesema itaingiza kipengele katika muswada wa fedha
kitakachowalazimisha wakurugenzi wa halmashauri nchini kutenga na kutoa
asilimia 10 ya mapato ya halmashauri hizo kwa ajili ya mikopo ya kina mama na
vijana.
Hayo yamesemwa leo Bungeni jijini Dodoma katika kikao cha 43
mkutano wa 11 wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Naibu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Anthony Mavunde wakati akijibu swali la
Mbunge Viti Maalumu mkoani Mwanza, Kemirembe Lwota.
Kemirembe alihoji bungeni kuwa, serikali ina mpango gani
katika kuziwezesha halmashauri kutoa fedha za mikopo kwa wananchi, ambapo
alisema halmashauri nyingi nchini zimekuwa hazitoa fedha hizo.
Waziri Mavunde amejibu kuwa “Kuna kipengele kitaingizwa
kwenye muswada wa fedha ‘finance bill’ kitamlazimisha kila mkurugenzi hiki kiasi
cha fedha kinatengwa na kinatolewa, sasa hivi ni option kutolewa, lakini
kipengele hicho kikiingizwa kisipotengwa
watachukuliwa hatua za kisheria, tutaleta kipengele ili kuhakikisha fedha hizi
zinatengwa.”
