Kiwanda chatuhumiwa kueneza hewa ya sumu Dar


WATU wawili wameathirika vibaya na wengine zaidi ya 42 kukimbilia hospitali muda mfupi baada ya kuvuta hewa inayodaiwa kuwa ni ya sumu kutoka katika kiwanda cha sabuni cha Royal kilichopo Mabibo jijini Dar  es Salaam.
Hali  hiyo ilijitokeza Dar es Salaam leo baada ya mfumo a kuthibiti hewa chafu kushindwa kufanya kazi na kuleta taharuki kubwa miongoni mwa wananchi wanaoishi karibu na eneo hilo
Akizungumza kwa taabu katika Hospitali ya Sinza Palestina leo mmoja wa waathirika hao Rashid Hamad Madina amesema yeye aliamka asubuhi kama kawaida lakini ilipofika majira ya saa 2.30 asubuhi alijisikia vibaya .
Anasema baada ya kujisikia vibaya ghafla alianza kukohoa na mwisho kupiga chafya mfululizo ambapo baadaye alianza kupata shida ya kupumua na ndipo alipoamua kwenda kiwandani kuwaeleza  kwa kuwa haishi mbali na kiwanda hicho
“Nilijisikia vibaya sana na wakati nilipokuwa naelekea kiwandani huku nikikohoa kwa shida nilijikuta nikianguka chini na nilipozinduka nilijikuta nipo hapa hospitali Sinza”alisema Hamad.
Hamad aliongeza kuwa suala la  kuvuta harufu mbaya kutoka katika kiwanda hicho ni la kawaida kwa kuwa hutokea mara kwa mara lakini hilo lililotokea safari hii ni kubwa zaidi.
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Kisale Makori alithibitisha kutokea kwa tukio na kuahidi kuchukua  hatua  baada ya kufanya uchunguzi .
“Ni kweli tukio hilo limetoka lakini watu walioathirika zaidi ni watu wawili ambao wapo katika hospitali ya Sinza ila mmoja ameruhusiwa na amebaki mmoja lakini kuna watu 42 waliokwenda hospitali pale Mabibo  jeshini kuangalia kama wameathirika juu ya tukio hilo”anasema Makori

Post a Comment

Previous Post Next Post