Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam imewaongeza Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Pope na mkandarasi wa uwanja wa timu hiyo, Frank Peter Lauwo, katika kesi ya utakatishaji fedha inayowakabili Rais wa timu hiyo, Evans Aveva na makamu wake, Geofrey Nyange 'Kaburu'.
Mahakama hiyo imeagiza Hans Pope na Lauwo wafikishwe mahakamani kujibu mashitaka hayo yanayowakabili ambapo amri hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba baada ya washitakiwa hao kutafutwa bila mafanikio na kuomba hati ya kuwakamata.
Kufuatia mabadiliko hayo washtakiwa hao wamesomewa upya hati ya mashtaka na sasa wanakabiliwa na mashtaka 10 tofauti na hati ya awali iliyokuwa na mashtaka matano.
Kesi hiyo imahirishwa hadi Mei 14, 2018 kwa ajili ya kutajwa na kufuatilia kama washitakiwa hao wawili watakuwa wamekamatwa.
