Bungeni ni moto, Ndugai awa Mbogo


SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, ameonyesha kutoridhishwa na majibu ya swali lililohusu suala la sukari ambalo aliagiza liulizwe tena bungeni wiki iliyopita.

Ndugai alitoa kauli hiyo jana bungeni wakati swali la Mbunge wa Baraza la Wawakilishi, Jaku Hashim Ayoub, lilipokuwa limejibiwa na Naibu Waziri Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Stella Manyanya.

“Swali hili mtakumbuka ni mwendelezo wa lile swali nililosema lirudiwe wiki iliyopita ukisoma swali na majibu ni vitu viwili tofauti. Niseme tu kwa leo inatosha tuvuke hapo tuendelee na mambo mengine,” alisema.

Katika swali lake, Jaku alisema kumekuwapo na viwanda vingi vya sukari nchini lakini bado kumekuwa na uhaba mkubwa wa bidhaa hiyo hususan upande wa Tanzania Bara na kumekuwapo na utofauti wa bei.

“Mfano bei ya mfuko wa kilo 50 ni Sh.65,000 kwa upande wa Zanzibar ambako kuna kiwanda kimoja tu cha sukari, lakini Tanzania Bara mfuko huo wa kilo 50 huuzwa kwa 120,000,”alisema.

Kutokana na tofauti hiyo, alihoji kuna tatizo gani linalofanya sukari iuzwe bei ya juu kiasi hicho kwa upande wa Tanzania Bara.

“Je, serikali itachukua hatua gani ili kuwapatia wananchi unafuu katika upatikanaji wa bidhaa hiyo na kwa upande wa Zanzibar katika kipindi ambacho matumizi ya sukari kwa wananchi yanaongezeka. Mfano mwezi wa Ramadhan, serikali inashusha ushuru wa kuingiza nchini ni kwa nini utaratibu huu usizingatiwe?” alihoji.

Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri Manyanya alisema ukaguzi wa maofisa masoko katika masoko ya Dar es Salaam na Zanzibar unaonyesha kuwa bei ya sukari kwa gunia la kilo 50 ni Sh. 101,000 hadi Sh.105,000 kwa Dar es Salaam na Sh.71,000 hadi Sh. 77,000 kwa Zanzibar.

“Mapitio ya bei hizo na kama Mbunge alivyoeleza kwenye swali hili kipengele (c) tofauti ya bei katika eneo la Dar es Salaam na Zanzibar kwa kiasi kikubwa inatokana na utozaji wa ushuru na kodi,” alisema.

Hata hivyo, alisema inaonekana dhahiri kuwa kiasi cha kodi kinachotozwa kwenye gharama ya mfuko wa kilo 50 Zanzibar ni kidogo wakati Dar es Salaam ushuru na kodi ni asilimia 25 na 18 vyote kwa pamoja.

Alibainisha viwanda vya sukari nchini kwa wastani vinazalisha tani 320,000 kwa mwaka wakati mahitaji ya sukari ya mezani ni tani 455,000.

“Chini ya utaratibu maalum serikali huagiza upungufu katika uzalishaji ili kutosheleza mahitaji ya soko, Katika kipindi hiki (Februari-Mei) viwanda vyetu vimefungwa kwa ajili ya matengenezo na kupisha msimu wa mvua za masika,”alisema.
Manyanya alisema tani 135,000 zimeagizwa kuziba pengo na sehemu kubwa ya shehena hiyo imeshawasili nchini.

Aidha alisema chini ya utaratibu maalum wa kulinda na kuhamasisha viwanda vya sukari ni viwanda vya sukari nchini vinaruhusiswa kuagiza upungufu wa sukari.
“Utaratibu wa wenye viwanda unaambatana na masharti ya kupanua mashamba na viwanda vyao ili katika kipindi cha miaka mitatu tuwe na uzalishaji wa kutosha mahitaji ya ndani na kuuza ziada nje,”alisema.
Manyanya alisema zimeagizwa tani 135,000 ili kuhakikisha kuwa wanakidhi mahitaji ya soko.
“Kulingana na Sheria za Kodi kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, sukari inayoagizwa toka nje ya jumuiya hutozwa ushuru kwa asilimia 100 na asilimia 18 ya gharama (CIF) ila kwa kulenga kuwapa unafuu walaji, sukari hapo juu inatozwa kwa kiwango cha asilimia 25 na asilimia 18 ya gharama,” alisema.

Post a Comment

Previous Post Next Post