Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo Zitto Kabwe ametumia siku ya kuzaliwa ka Rais wa awamu ya pili Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi kwa kumbusha namna alivyowajibiki kipindi akiwa waziri kwenye kashfa mauaji ya MWASHI.
Zitto ameikumbuka Tarehe 22 Januari mwaka 1977 ambao Mwinyi alikuwa Waziri wa mambo ya ndani aliwajibika kujiuzulu kutokana na mauaji hayo
soma hapa waraka wa Zitto aliotumia kwenye kumtakia kheri ya kuzaliwa kwa Rais huyo mstaafu
HAPPY BIRTHDAY MZEE MWINYI
Mauaji ya MWASHI na MKIRU: Mafunzo ya Maisha ya Viongozi Waliojali Utu na Haki
[Tafakuri ya Kabwe Z. Ruyagwa Zitto Juu ya Kumbukumbu ya Miaka 93 ya Kuzaliwa kwa Rais Ali Hassan Mwinyi]
Januari 22, 1977 aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, ndugu Ali Hassan Mwinyi, aliweka rekodi ya Uwajibikaji nchini, kwa kujiuzulu nafasi yake, kwasababu ya mauaji na vitendo vya mateso yaliyofanywa na Vyombo vya Ulinzi na Usalama dhidi ya wananchi wa Mikoa ya Mwanza na Shinyanga (Mauaji ya MWASHI), vitendo vinavyofanana sana na mauaji yaliyofanyika eneo la MKIRU (Mkuranga - Kibiti - Rufiji) katika Mkoa wa Pwani.
Juzi, Mei 4, 2018 nilitoa hotuba bungeni, nikichangia hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, katika mchango huo nilitia orodha ya Watanzania wenzetu 68 wanaotajwa kuuawa na Vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama huko MKIRU (Mkuranga - Kibiti na Rufiji) pamoja na kueleza juu ya uwepo wa Taarifa za mauaji na kupotea kwa zaidi ya watu 380, na hivyo nikaliomba Bunge liridhie kuunda Kamati Teule ya kuchunguza jambo hilo la kinyama kwa wananchi wenzetu.
Na si mimi tu ndiye niliyetoa maelezo juu ya kuuawa na kupotea kwa watu Nchini, wabunge wengi wamefanya hilo, akiwemo Mbunge wa Arusha Mjini, ndugu Lema, na Mbunge wa Kilwa Kusini, ndugu Bungara ‘Bwege’ aliyeelezea kwa hisia kadhia ya mauaji, kuteswa, kupotea na kutiwa ukilema kwa wananchi waliovamiwa na kukamatwa na Vyombo vya Ulinzi na Usalama katika Msikiti wa Chumo huko Kilwa.
Ni bahati mbaya kuwa Bunge lilikataa kuunga mkono hoja ya kuchunguza jambo hili la kinyama walilofanyiwa watanzania wenzetu, Serikali ya CCM ikionekana kutokujali kabisa uhai wa watu wake, na ikikataa uchunguzi ambao ungeonyesha ukweli, na kurudisha matumaini ya kupata HAKI kwa Watanzania wenzetu.
Kwa lengo la kunifariji, mmoja wa Wazee wetu wastaafu, ambaye alikuwa Waziri wakati wa Mauaji ya MWASHI (Mwanza - Shinyanga) alinipa barua [ Hii hapa chini ] ya Mzee Ali Hassani Mwinyi, akionyesha kusikitishwa kwake na hatua ya Bunge kukwepa wajibu wake wa kuchunguza mauaji ya raia, na zaidi akihuzunishwa na namna Serikali ya sasa isivyojali juu ya matendo ya ukatili wa vyombo vya Ulinzi na Usalama dhidi ya raia.
Barua hii inaonyesha namna misingi ya ujenzi wa Tanzania yetu ilivyojikita kwenye Haki, Ukweli, Utu, Sheria na Viongozi kuwaheshimu wananchi wanaowaongiza, inaonyesha namna Viongozi wanaojali Utu wa Watu walivyoenenda wakati matukio ya mauaji dhidi ya raia yalipotokea huko nyuma. Ni barua iliyopaswa kuwa mwongozo wetu Viongozi wa sasa, wa kutupa Dira na mwelekeo wa namna ya kuwaongoza watu wetu katika misingi iliyoasisi Taifa letu.
Na mzee Mwinyi hakupungua kitu kwa unyenyekevu na uwajibikaji huu aliouonyesha kwa Watanzania, aliweka msingi wa Haki kutendwa kwa wananchi walionewa, akatoa ukumbusho wa vyombo vyetu vya Ulinzi kuenenda kiutu na kwa kufuata sheria bila kuonea watu, na akasimika msingi imara wa ujabikaji kwa viongozi wenye dhamana ya kuhakikisha usalama wa wananchi.
Kwa kitendo hiki, mzee Mwinyi alirudisha matumaini ya wananchi kupata haki, na akajenga heshima na imani kubwa kwa viongozi na wananchi wenzake. Ndio maana haikushangaza kuwa miaka kadhaa tu baada ya kujiuzulu, alipewa tena nafasi ya kuwaongoza wananchi wenzake, mara hii nafasi kubwa zaidi, kwanza akiwa Rais wa 3 wa Zanzibar (1984 - 1985), kisha akiwa Rais wa 2 wa Tanzania.
Barua yake hii ya Unyenyekevu, na inayoonyesha Utu na Kujali ni historia njema ya Utaifa wetu (Taifa linajali Utu na kusimamia haki za wanyonge na wanaoonewa), ni urithi (legacy) mwema wa Uongozi wake kwa Taifa letu. Viongozi wa sasa hatuna budi kuiga mema haya ya viongozi waliotutangulia.
Leo wakati tukiadhimidha miaka 93 tangu kuzaliwa kwa kwa mzee Ali Hassan Mwinyi tuwatafakari mamia ya wananchi wenzetu waliouawa, kuwa vilema na hata kupotea huko MKIRU, tuwatafaki ndugu na jamaa zao, namna wanavyoumizwa na hali hii, na namna walivyopoteza matumaini ya kupata Haki na kuujua ukweli wa walipo ndugu zao. Tafakari husika itusaidie kujirudi na kujisahihisha, ili tutende haki kwa watu wa MKIRU.
Mola ampe afya njema mzee Mwinyi, ampe umri mrefu zaidi ili tupate hekima, busara, uzoefu na nasaha zake.
Happy Birthday Mzee Mwinyi
Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Mbunge, Kigoma Mjini
Kiongozi wa Chama, ACT Wazalendo
Mei 8, 2018
—-Barua ya Mzee Mwinyi Kujiuzulu —-
Telegram “Usalama”
Januari 22, 1977
Mheshimiwa Mwalimu J. K. Nyerere
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ikulu
Dar es salaam
Mwalimu,
KUJIUZULU
Hivi karibuni, kiasi cha miaka miwili iliyopita palizuka vikundi flani vya wauaji, katika mikoa ya Mwanza na Shinyanga. Idadi kubwa ya wananchi wakiuliwa hovyo kila mwezi kwa visingizio vya uchawi na vinginevyo. Serikali ililazimika kuyamaliza maovu hayo kwa nia njema ya kuzuia hali hiyo isiendelee, na pia kuwajua wahalifu hao ili wakamatwe na wafikishwe mahakamani.
Katika kutekeleza nia nzuri ya Serikali, vyombo vinavyohusika na utekelezaji, Polisi ikiwemo, vilivuka mipaka ya wajibu wao, na vikajipa madaraka ya kuogelea kwenye vitendo viovu vya Kishenzi, Kinyama na Kikatili, hata baadhi ya watu waliokamatwa kwa kushukiwa tu kwamba wanahusika wakafa na wengine wakapata vilema vya kudumu.
Polisi ni chombo cha kulinda amani, mali na maisha ya watu wake; si chombo cha kuwaua. Pia Polisi ni chombo cha kuhifadhi na kudumisha usalama na haki; si chombo cha kudhulumu, kuonea na kuwatesa makusudi wananchi wananchi wale wale wanaokigharamia kukiweka. Kwa bahati mbaya maovu kama haya ndiyo hasa yaliyotendwa na vyombo vya Serikali huko Mwanza na Shinyanya.
Kijinai, mimi binafsi nisingehusika, kwani sikushiriki wala sikushauri, sikuagiza wala kuelekeza kwamba mambo yafanywe kama hivyo yalivyofanywa. Kwa kweli hata mimi nilifichwa, kwani niliarifiwa baada ya tume yako kuteuliwa.
Hata hivyo, Kisiasa nakiri kuwa nahusika, siwezi kukwepa kwa sababu dhamana yangu ya Uwaziri (na Mambo ya Ndani) inaambatana na wajibu unaonitaka nijue yanayotendeka Wizarani na pia niweze kudhibiti na kuhakikisha mwenendo mwema wa Jeshi la Polisi.
Msahafu unatuusia kwa kusema; “wala hatabeba (dhambi) mbebaji, mzigo (wa dhambi) wa (Mtu) mwengine”. Kisiasa mzigo huu ni wangu, na nakubali kuubeba kwani hakuna mwengine wa kuubeba.
Kwa hiyo, Mwalimu, nakuomba mambo matatu. Kwanza naomba radhi mimi nafsi yangu (binafsi) na pia naomba radhi kwa niaba ya askari wote walio wema. Pili, naomba vilevile uelewe sehemu yangu katika kosa hili. Tatu, kwa fedheha hili, naomba unikubalie kujiuzulu.
Wako Mtiifu
H. Mwinyi (Mbunge)
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi
