Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi-CCM Taifa- NEC imemuachisha
uanachama Mwakilishi wa Jimbo la Jang’ombe liliko visiwani Zanzibar, Abdallah
Diwani, pamoja na kutoa karipio kwa wajumbe wa Bunge la Afrika Mashariki-EALA, Fancy
Nkuhi na Mariam Ussi Yahya.
Adhabu hizo zimetolewa leo na Wajumbe wa NEC katika kikao
chake kilichofanyika leo Mei 29, 2018 jijini Dar es Salaam baada ya wajumbe hao
kuazimia kuwaadhibu makada hao wa CCM.
Sehemu ya taarifa iliyotolewa kwa umma na Katibu wa Itikadi
na Uenezi, Humphrey Polepole, inaeleza kuwa Diwani ameachishwa uanachama kwa kosa la
kwenda kinyume na miiko ya uongozi wa CCM.
Wakati Nkuhi na Mariam Yahya ambao ni wajumbe wa EALA
wamepewa karipio kali kwa kosa la kuwa na mwenendo usioridhisha na kulinda
maslahi ya nchi unaokinzana na misingi na miiko ya uongozi.
Wajumbe hao wa EALA wamewekwa chini ya uangalizi wa
kimaadili kwa muda wa miezi kumi na nane.
