Chama cha Act-Wazalendo kinatarajia kufanya uchaguzi wa
viongozi wa kitaifa katika chama hicho ili kuimarisha muundo wake kuelekea
maandalizi ya ushiriki wa uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika
mwakani, na uchaguzi mkuu wa 2020.
Taarifa hiyo imetolewa leo Mei 27, 2018 na Katibu wa Itikadi
na Uenezi Act, Ado Shaibu wakati akizingumza na wanahabari jijini Dar es
Salaam.
Ado amesema viongozi wanaotarajiwa kuchaguliwa kwenye
uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika jijini Mbeya mwishoni mwa mwezi Agosti
mwaka huu, ni kiongozi wa chama, mwenyekiti wa chama taifa, makamu wenyeviti wa
bara na Zanzibar na wajumbe wa kamati kuu.
“Tulisema 2018 pamoja na mambo mengine utakuwa mwaka wa
kuimarisha muundo wa chama kupitia uchaguzi, zoezi la uchaguzi linaendelea
vizuri lipo katika ngazi ya majimbo kwa sasa, na hivi karibuni tutaingia ngazi
ya mikoa, uchaguzi wa viongozi ngazi ya kitaifa utafanyika mwishoni mwa agosti
kwa kuanzia 25 hadi 27,” amesema Ado na kuongeza.
“Viongozi wanaopaswa kupatikana kupitia uchaguzi, ni kiongozi
wa chama, makamu mwenyekiti Zanzibar na bara, wajumbe wa kamati kuu hawa wote
wanapatikana kupitia uchaguzi, katiba inasema uchaguzi unatakiwa kufanyika kila
baada ya miaka mitano lakini kutokana na sababu mbalimbali utafanyika mwaka huu
ikiwa ni miaka mitatu imepita tangu viongozi kuchaguliwa, ili tujiandae chaguzi
zijazo.”
