Takriban watu saba wamekamatwa mjini Arusha nchini wakihojiwa kuhusiana na majukumu yao katika maandamano ya kisiasa dhidi ya serikali mnamo tarehe 26 Aprili ambayo ni siku ya muungano.
Kaimu kamanda wa polisi Arusha, Yusuph Ilembo aliwaambia waandishi siku ya Jumanne kwamba kukamatwa kwa watu hao saba ni kunafuatia uchunguzi uliofanywa na polisi.
Majina yao hayakuweza kuwekwa wazi lakini kulingana na Kamanda Ilembo wengine wao ni wanafunzi wa chuo kikuu.
''Kama serikali hatutasita , maandamano haya ni haramu hatutakubali kuhangaishwa na watu wachache ambao wanataka kuharibu amani ya Tanzania'', alisema afisa huyo.
Kukamatwa kwao kunajiri saa chache baada ya serikali ya Uingereza kutoa agizo la tahadhari kwa raia wake wanaoelekea Tanzania ikidai kuwa uwezekano wa maandamano ya kisiasa nchini humo wakati wa siku kuu ya muungano unaweza kusababisha maafa.
Mwanaharakati wa mitandao ya kijamii anayeishi nchini Marekani kutoka Tanzania, Kimambi ametoa wito wa kufanyika kwa maandamano dhidi ya serikali mnamo tarehe 26 Aprili kwa kile anachodai ni ukandamizaji wa uhuru wa kisiasa na haki za kibinaadamu.
Serikali tayai imepinga madai hayo na kusema kuwa maandamano hayo yatakuwa kinyume na sheria.
Kwa upande wake, rais wa Tanzania John Pombe Magufuli kwa mara kadhaa amesema hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wale ambao watashiriki maandamano hayo.
Mwezi Machi mwaka huu, Polisi mjini Dodoma waliwashikilia watu wawili kwa kosa la kuhamasisha maandamano kwa njia ya mitandao.
Polisi iliwataja watu hao kuwa dereva na mkulima, ambao waliwawashutumu kwa kutumia mitandao ya kijamii kuhamasisha maandamano yanayopangwa kufanyika tarehe 26 April mwaka huu
Sikiliza mahojiano kati ya Mwandishi wa BBC, Sammy Awami na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Gilles Muroto na kwanza alianza kwa kumuuliza undani wa kukamatwa kwa vijana hao.

