Yondani: Tupo fiti kufuzu Kombe la Shirikisho


Beki wa kati wa Yanga, Kelvin Yondani, ameta­mba kuwa wapo fiti na watahakikisha wanafu­zu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Yanga leo saa 10:00 jioni watajitupa uwanjani kuvaana na Welayta Dicha ya Ethiopia katika mchezo wa marudiano kwenye Uwanja wa Hawass uliopo Awassa, Ethiopia.

Katika mechi ya kwanza jijini Dar es Salaam, Yanga ilishinda mabao 2-0 hivyo kujiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele katika michuano hiyo.
 

Yondani ambaye aliukosa mchezo uliopita kutokana na kuwa na kadi mbili za njano, alisema hawatakubali kuondolewa katika michuano hiyo.

Yondani alisema, walijifunza kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kutolewa na Township Rollers ya Botswana, hivyo sasa hawataki kurudia makosa.

“Ushindi wa mabao 2-0 tulioupata nyumbani umetuongezea hamasa kubwa sisi wachezaji, hivyo kesho (leo) tutaingia uwanjani tukiwa na mtaji wa mabao mawili ambayo tumeahidi kuyalinda ugenini.

“Tumedhamiria na tutahakikisha tunapata matokeo yatakayotuwezesha kutinga hatua ya makundi na hilo linawezekana kabisa kwani kila mchezaji anajua umuhimu wa mchezo huu.

“Hivyo, tutapambana dakika zote 90 kuhakikisha tunafanikiwa matokeo mazuri yatakayotupeleka hatua ya makundi, hivyo mashabiki wa Yanga waondoe hofu,” alisema Yondani.

Post a Comment

Previous Post Next Post