Lema aachiwa huru, akamatwa afunguliwa kesi upya


Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema amefikishwa mahakamani tena mchana wa leo, April 27, 2018 na kusomewa kosa moja la kuamsha hisia kwa njia isiyohalali kinyume cha sheria.

Hii ni baada ya Lema kuachiwa huru mapema leo na Mahakama ya wilaya (Sekei) baada ya upande wa Jamhuri kuondoa mashtaka yaliyokuwa yakimkabili baada ya serikali kudai haina nia ya kuendea.

Hata hivyo baada ya kutoka mahakamani alipokeawito kutoka kwa mkuu wa upelelezi wa polisi mkoa wa Arusha akitakiwa kufika katika mahakama ya hakimu mkazi, Arusha ambapo alisomewa shtaka hilo.

Mbele ya hakimu, Nelson Baro mwendesha mashtaka wa serikali, Eliainenyi Njiro aliieleza mahakama hiyo kwamba, mshtakiwa Lema, mnamo tarehe 22 Oktoba mwaka 2016 katika eneo la kambi ya Fisi ndani ya Jiji la Arusha alitamka maneno yenye kuamsha hisia isiyo halali.

Maneno hayo ni "Rais Magufuli akiendelea na tabia ya kudhalilisha demokrasia na uongozi wa upinzani iko siku taifa litaingia kwenye umwagaji wa damu.

“Rais yeyote ambaye haheshimu mipaka ya sheria, mipaka ya Katiba, Rais huyo  ataingiza taifa katika majanga na umwagaji damu, watu watajaa vifua, wakiamua kulipuka polisi hawa wala jeshi halitaweza kudhibiti uhalifu utakaojitokeza.”

Hata hivyo mshtakiwa Lema alikana shtaka na upande wa jamhuri ulidai hauna pingamizi la dhamana, jambo ambalo mshtakiwa alikidhi sharti la dhamana kwa mdhamini mmoja aliyesaini bondi ya shilingi za kitanzania milioni tano.

Hakimu Baro aliahirisha shauri hilo hadi Mei 30 mwaka huu itakapokuja kwa ajili ya kutajwa baada ya upande wa Jamhuri kudai upelelezi bado haujakamilika.

Kesi hiyo ni namba 132 ya mwaka 2018.

Post a Comment

Previous Post Next Post