Trilion 1.5 za CAG 'zapigwa danadana', mitandao yahusishwa

Mjadala kuhusu kupotea kwa fedha jumla ya trilioni 1.5 umechukua sura mpya baada ya Rais Dk. John Magufuli kuwasimamisha Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango kueleza kuhusu ukweli wa swala hilo.
Maofisa hao wa serikali waliposimama walikanusha kuwa hakuna upotevu wa fedha hizo ambazo kwa siku kadhaa kumekuwepo mjadala mkali kuhusu kile kinachodaiwa kuwa ofisi ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali ilibaini utata kuhusu matumizi ya pesa hizo ambazo ni sawa na dola za kimarekani milioni 650.


Wakati mwanasiasa wa upinzani Zitto Kabwe akitaka ufafanuzi kutoka serikalini kuhusu matumizi ya fedha hizo, viongozi wa chama tawala, CCM na serikali wamekuwa wakisisitiza kwamba hakuna upotevu wowote wa fedha hizo uliotokea.
Mapema jana Aprili 20 katika hafla ya kuwaapisha majaji wapya Ikulu, Dar es Salaam, Rais Magufuli alisema kinachoendelea kwa sasa ni upotoshaji wa makusudi kwa umma kuhusu sakata hilo.
'Siku moja nikampigia CAG mbona kwenye ripoti yako uliyonisomea hapa Ikulu hukunieleza huu wizi wa trilioni 1.5? kwa sababu ungenisomea hapo siku hiyohiyo ningefukuza watu, kama nimefukuza wakurugenzi watatu siku hiyo hiyo kwa sababu ya hati chafu, hawa wa trilioni 1.5 uliwaficha wapi? kwenye ripoti yako sioni, Profesa Assad akaniambia hakuna kitu kama hicho nikamuuliza Katibu Mkuu akasema hakuna kitu kama hicho''. alisema rais Magufuli.
Rais Magufuli amesema hali hii inatokana na uhuru wa watu kusema au kuweka chochote wanachokitaka mitandaoni. Ameonya kwamba hali hii ikiendelea madhara yake kwa taifa ni makubwa.
''Kuna ugonjwa tumeupata watanzania wakufikiri kila kinachoandikwa kwenye mitandao ni cha kweli, lakini ni kwa sababu hii mitandao hatui-control sisi wapo watu ambao kazi yao ni kutengeneza biashara'', alisema Rais Magufuli.
Amevitaka vyombo vya sheria kushughulikia kesi za upotoshaji haraka pamoja na kuiachia kamati ya bunge ya hesabu za serikali (PAC) kufanya uchunguzi wake.

Post a Comment

Previous Post Next Post