MWANAFUNZI wa kidato ya pili katika Shule ya Sekondari ya Mang’oto, wilayani Makete mkoani Njombe, Esau Msigwa (15), ambaye alichoma bweni la shule hiyo amehamishwa shule hiyo na mzazi wake kutakiwa kulipa faini ya Sh. milioni nane.
Mwanafunzi huyo alichoma bweni hilo Machi 13, mwaka huu, baada ya wanafunzi wenzake kumpa adhabu kutokana na tabia yake ya wizi.
Akihojiwa na Nipashe, Mkuu wa Wilaya ya Makete,Veronica Kessy, alisema baada ya tukio hilo mhusika alishtakiwa kwa mujibu wa sheria za mtoto.
“Mzazi aliambiwa achangie fidia ya kusaidia kujenga bweni na mwanafunzi huyo alipatiwa kifungo cha nje cha miaka mitatu pamoja na kutakiwa kuhama shule,” alisema Kessy.
Nipashe ilizungumza na Mratibu wa Elimu Kata ya Mang’oto, Furaha Kiando, ambaye alisema tayari adhabu imetolewa kwa mwanafunzi huyo na kwamba mzazi wake atawajibika kumpeleka shuleni hapo kwa ajili ya kufanya mtihani wa kidato cha pili tu.
“Amepewa adhabu ya kulipa fidia ya uharibifu pamoja na kuhamishwa shule ila kwa sababu amesajiliwa kufanya mtihani wa kidato cha pili shule hii atafanya mtihani akiwa chini ya ulinzi na mzazi wake atakuwa anamleta na kumrudisha,” alisema.
Kiando alisema mwanafunzi huyo aliiba pipi, biscuit na karanga kwenye kibanda cha mwalimu shuleni hapo na wanafunzi wenzake waligundua kuwa ndiye anahusika na wizi huo.
“Wanafunzi wenzake walimuona akiwa anakula kwa kujificha wakati wakitoka kujisomea usiku na wakati wanapoingia kulala walikuwa wanamuona anavyojifunika na blanketi, wakamfuatilia na kugundua kuwa huwa anaiba vitu hivyo kwenye duka la mwalimu,” alisema na kuongeza:
”Sasa walipogundua walimpa adhabu ya kuruka kichura chura huku wakimweleza anawaharibia sifa shuleni hapo, adhabu hiyo hakuipenda akaanzisha visa na wenzake walipokwenda kujisomea alishusha magodoro yao na kuyachoma hali iliyosababisha bweni nzima kuungua,” alisema.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mang’oto, Mengi Chalamila, alisema sababu za kuchoma bweni hilo ni hasira zilizotokana na adhabu aliyopewa na wanafunzi wenzake kutokana na tabia yake ya wizi.
Chalamila alisema baada ya kuripotiwa kwa tukio hilo taratibu mbalimbali zilifanyika na ndipo alipohamishwa shule na mzazi wake kutakiwa kulipa fidia hiyo.
Alisema moto huo umesababisha hasara kubwa na kwamba jengo aliloliunguza lina thamani ya Sh milioni 80, vitanda vyenye thamani ya Sh. milioni 5.7, vitabu vyenye thamani ya Sh. milioni 6.6 na vifaa mbalimbali vya wanafunzi vyenye thamani ya Sh. milioni 21, hivyo jumla ya hasara ni Sh. milioni 102.7
Baba mzazi aomba apunguziwe fidia
Baba wa mwanafunzi huyo ambaye ni mwalimu katika Shule ya Msingi ya Makangarawe, Aldo Msigwa, alisema amesikitishwa na tukio lililofanywa na mtoto wake huku akiomba apunguziwe fidia.
Alisema kutokana na uzito wa jambo hilo ilimlazimu kwenda kukopa hela na kupeleka Shilingi milioni tano juzi shuleni hapo ambazo zimekwenda kusaidia ujenzi wa bweni.
“Hili tukio sikulifanya mimi ingawa ninaumia sana ninaomba wanisaidie kunipunguzia hiyo fidia maana siko vizuri kiuchumi na bado nina watoto wengine ninawasomesha hata huyu sijui kama nitampeleka tena shule maana ada sijui kama nitaipata,” alisema.
“Kama unavyoelewa maisha yetu ya huku kijijini kuambiwa utoe Sh. milioni nane ni shida sana, niliomba nitoe hii fidia angalau kwa awamu, lakini nilikataliwa hali ya uchumi kila mtu anaijua,” alisema.
