Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Wallace
Karia ameipongeza klabu ya Yanga
baada kufanikiwa kutinga katika hatua ya
Makundi Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Yanga wamefuzu katika
hatua hiyo kwa ushindi wa jumla wa mabao 2-1 baada ya mchezo wa awali kushinda kwa mabao 2-0 kabla ya kufungwa bao 1-0 walipokuwa
ugenini dhidi ya Welayta Dicha ya Ethiopia.
Rais wa TFF, Karia ametoa
pongezi hizo kwa niaba ya TFF baada ya Yanga kufanikiwa kutinga katika hatua hiyo na ikiwa ni timu pekee
inayoiwakilisha Tanzania katika michuano
hiyo, baada ya wekundu wa msimbazi Simba kuondoshwa katika michuano hiyo.
Yanga wameingia nchini usiku wa jana,wakitokea Ethiopia na
kulakiwa na baadhi ya washabiki waliojitokeza kuwapokea, kesho Yanga watafunga safari kuelekea Mbeya kwa ajili ya mchezo wao wa Ligi Kuu Bara, dhidi ya wenyeji wao Mbeya City, mchezo utakaorindimwa katika
uwanja wa Sokoine mijini Mbeya.
Droo ya michuano hiyo itafanyika kesho Aprili 21, katika makao makuu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika
(CAF) Cairo, nchini Misri kuanzia majira ya Saa 8:00 mchana.
Na usiku wa leo
meneja wa Yanga, Hafidh Kido, anatarajia kwenda nchini Misri kuiwakilisha Yanga
katika droo hiyo.
