Mwenyeki wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Freeman Mbowe na viongozi wengine watano wameshikiliwa na jeshi la Polisi leo Machi 27, 2018 baada ya kuwasili kituo cha Polisi cha Kati Dar Es Salaam kuitikia wito wa polisi ikiwa ni muendelezo wa kufanya hivyo kila wanapohitajika kwa kutimiza masharti ya dhamana.
Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Idara ya Mawasiliano na Habari wa chama hicho kupitia ukurasa wa Twitter, Tumaini Makene amesema:
"Viongozi Wakuu wa Chama pamoja na wabunge waliokuwa wameripoti Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalum ya Dar wakitimiza masharti ya dhamana yao, wamewekwa mahabusu.Polisi hawajaeleza sababu ya kufanya hivyo.Mawakili wanashughulikia. Tutaendelea kuwapatia taarifa"
Kwa mujibu wa taarifa hizo, viongozi hao wamefutiwa dhamana yao kwa maelekezo ya Mkuu wa Upelelezi Makosa ya Jinai Kanda Maalum ya Dar es Salaam (ZCO) huku jeshi hilo likidai kuwa watafikishwa mahakamani Jumatano, Machi 28, mwaka huu.
Viongozi wengine waliowashikiliwa na Polisi ni Katibu Mkuu Dkt. Vicent Mashinji, Naibu Katibu Mkuu Bara John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Salum Mwalimu, Peter Msigwa na Mbunge Ester Matiko.
